Miiko ya kazi ya uchungaji
Na Pr.Filbert Mwanga
Kazi ya uchungaji ni kazi nyeti tena ya muhimu sana katika jamii yoyote. Unapoitwa mchungaji umebeba jina ambalo ni la heshima kupita Rais wa nchi. Hivyo jamii yoyote unapotamka kuwa wewe ni mchungaji wanaanza kupiga picha mtu ambaye ni mtakatifu asiyeweza kukutwa na tuhuma yeyote na pia asiyekosea. Hivyo ijapokuwa ni dhana iliyojengeka kwa jamii bado yatupasa kuiheshimu dhana hiyo kwa kuzingatia miiko ya kichungaji. Yapo mambo ya msingi wewe kama mchungaji unapaswa kuzingatia.
Miongozo yetu ya kanisa [Church Policy, Church manual, Ministers Manual, Pastoral Ministry, Elder’s Handbook, n.k.] imeweka wazi mambo ya msingi ambayo yanaweza kukuongoza (kukupa ‘Guideliness’) nini cha kufanya au usifanye (Dos and Don’ts).
1. Mchungaji unapaswa utambue kuwa umeitwa katika utumishi na wala sio ajira (It is a call but not a career) hivyo hutazamiwa kukutwa kwenye mgomo wowote kwa mambo ambayo hukubaliana nayo kama vile mshahara hautoshi, kugomea maagizo ya uongozi, au kuendesha migomo kwa washiriki dhidi ya uongozi wa ngazi za juu kwa jambo lolote ambalo hujaliafiki. Maana ya “wito ni kwa kawaida unaanza kwa shauku ya kujali hali ya kiroho ya wengine na kuhubiri neno la Mungu"
2. Mchungaji unapaswa kutambua kuwa umeitwa kwa ajili ya injili na wala sio kwa ajili ya cheo au kitu chochote. Hivyo hupaswi kutazamia swala la kupanda cheo au kufanya kampeni kwa ajili ya kupanda cheo.
3. Mchungaji hupaswi kuwa na tuhuma yoyote ambayo italeta aibu kwa kanisa au taaluma yako. Tuhuma hizi ni pamoja na Uasherati, Uzinzi, wizi wa fedha, n.k.
4. Epuka kutembelea washiriki walio wa jinsia tofauti na wewe nyakati za usiku au mahali ambapo hakuna watu mkiwa peke yenu. Usijaribu kutembelea wajane, wasichana, au waliotelekezwa peke yake bila mzee wa kanisa au shemasi mkuu wa kiume au mke wako.
5. Mchungaji epuka madeni kama ukoma kutoka kwa washiriki au watu ambao sio waumini au mashirika yoyote. Rafiki wako wa karibu unapokuwa na shida ni ofisi yako ya Konferensi au mtendakazi mwenzako. Bali uwe mwaminifu kulipa kwa wakati.
6. Mchungaji unapaswa kutokuwa na makundi ndani ya kanisa au kwa watendakazi wenzako. Hili linamaanisha hupaswi kuligawa kanisa katika makundi yoyote. Jaribu kufanya kila linavyowezekana kuleta umoja hata kwa wale ambao hawapendi umoja au wasiokuafika kwa kazi yako na uongozi wako.
7. Mchungaji unapaswa kuwa mwalimu au muhubiri. Kinachotazamiwa kwa mchungaji ni kuwa mfundishaji zaidi kuliko kuwa mhubiri kwa ajili ya kuelimisha kanisa. “Usijaribu kuwa muhubiri bali uwe mtendakazi wa Mungu.”
8. Mchungaji unapaswa kuunga mkono programu zote za kanisa bila kuwa kinyume na program hizo. Epuka kupinga kwa njia yoyote mipango kutoka juu au jambo jipya ambalo hujalielewa. Fundisha mafundisho yote ya kanisa na kanuni zake.
9. Sukuma idara zote ndani ya kanisa bila kupendelea idara yoyote. Hili likiwa na maana kupenda idara zote kwa kuzihamasisha bila kuwakatisha tamaa viongozi wake makanisani.
10. Mchungaji unapaswa kuhudhuria mikutano ya kanisa kama vile maombi ya jumatano, kufungua sabato, na kufunga sabato, makambi, efoti, unapokuwa karibu na matukio hayo yote.
11. Mchungaji unapaswa kuheshimu kazi ya mchungaji mwenzako uliyempokea mtaa au ofisi. Usikubali kujadili madhaifu ya mchungaji mwenzako uliyempokea kwani kufanya hivyo unaharibu heshima ya kazi ya kichungaji. Epuka kudharau mipango yake aliyoacha bali unapaswa kuisapoti mipango yake mizuri kisha ingiza yako taratibu kwa hakika bila kukashifu yake unayoiona kuwa ni mibovu.
12. Mchungaji unapaswa kusimamia mabaraza yote ya uchaguzi kwa ajili ya kuchagua viongozi watakaokusaidia kazi yako kwa mwaka huo. Ni jambo la lazima na la muhimu labda itokee tu kuwa wewe ni mgonjwa ama unadharura ya muhimu sana. Lakini ni vizuri kuteua mtu anayeweza kuwakilisha vizuri ndani ya baraza hilo ama uruhusu wachague mwakilishi lakini uwe umejulishwa pendekezo hilo.
13. Mchungaji uwe kielelezo nyumbani kwako kwa kuwa na ibada ya asubuhi na jioni kwa familia yako. Nunua lesoni za watu wazima, na za watoto ikiwa wapo wadogo.
14. Mchungaji unapaswa kuwa wakili mwaminifu kwa kutoa zaka na sadaka, kuwahi kwenye vikao vya kanisa au matukio yoyote, na pia kuwahi ibada kanisani. Epuka kutoa muda wa kukutana bila kufika kwa wakati mliopanga pamoja au uliotamka watu kuhudhuria kama vile mabaraza ya kanisa, semina, na kazi za mikono za kanisa.
15. Epuka sana kutumia fedha za zaka na sadaka ya konferensi (‘trust fund’) bila idhini ya ofisi. Usijaribu kukopa kwa njia iwayo yote au kuendeshea miradi yako kwa madhumuni ya kurudisha baadaye.
16. Usichukue fedha ya kanisa kwa matumizi yoyote bila idhini ya kanisa lote yaani mashauri ya kanisa. Usiende kwa mhazini wa kanisa kuchukua fedha yoyote bila uongozi wa kanisa kujua au kukupatia. Fanya kazi yote kupitia kwa mzee wa kanisa.
17. Mchungaji unapaswa kupeleka taarifa kila mwezi na taarifa za robo kwa wakati ili kutoa taarifa kwa uongozi wa juu swala la utendaji wako wa kazi katika mahali unapofanya.
18. Mchungaji unapaswa kuepuka ukabila au ubaguzi wa jinsia au hadhi (wasomi na wasiosoma au matajiri na maskini au mlemavu na asiye mlemavu).
19. Mchungaji unapaswa kufurahia maisha uliyonayo na pia ishi maisha ya kawaida bila hofu. Usitake kufanana na wengine wakati uwezo huna utaingia katika madeni na chuki.
20. Mchungaji unapaswa uwe mwaminifu kwa watu na kwa Mungu. Hasa unapopewa fedha na ofisi jitahidi kutoa taarifa ya kweli kwa matumizi uliyofanya. Kumbuka jicho la Mungu linaona kila wazo na kila tendo.
21. Mchungaji epuka kile kinachoitwa ‘conflict of Interest’. Kitu kinachofuja muda wako wa kazi au kinachopingana au kushindana na huduma ya kichungaji kama vile biashara za masafa marefu, hospitali, duka la dawa, mradi wowote mahali ambapo kanisa nalo limeweka yake, uendeshaji wa miradi mikubwa kama vile shule, zahanati, viwanda, n.k.
22. Mchungaji hupaswi kujiunga na vikundi vya siri (secret society) ambavyo vipo ulimwengu katika kuendesha mipango ambayo ni ya uhalifu, na biashara mbaya. Pia kujihusisha na uchezaji wa michezo ya bahati nasibu kwa ajili ya kujinufaisha kimaisha au kimapato. Hii inamaanisha tuache kucheza michezo yote inayotupatia mapato ya aibu. Soma kitabu cha Mashauri Juu ya Uwakili.
23. Mchungaji unapaswa kuonyesha mfano mzuri kwa familia yako kwa kumfanya mwenzi wako kuwa msiri wako na tena mfariji wako. Hivyo magomvi na mahusiano mabaya dhidi ya mwenzi wako ni sumu ya kazi yako uchungaji.
24. Mchungaji unapaswa kuishi kwa kushabihiana na kile unachofundisha kulingana na msingi wa mafundisho ya imani yetu ya kanisa la Waadventista Wasabato. Epuka kutoa mafundisho mapya ambayo kanisa mahalia wanakuwa na mashaka nalo bila kutafuta msaada kutoka kwa ndugu walio watendakazi wenzako ili kujua msimamo wake.
25. Mchungaji unapaswa kila wakati kutafuta kupanda mafanikio. Unapaswa kutafuta kiwango cha juu katika kazi yako. Hii ndio siri ya mafanikio katika huduma yako.
26. Mchungaji hupaswi kujiamini mwenyewe kupita kiasi; kwani jambo hili limesababisha wengi kuwa na dharau kwa watendakazi wenzao, na tena kushindwa kushaurika mahali anapokosea.
27. Mchungaji unapaswa kumheshimu mchungaji uliyepewa kama msimamizi wa kazi anayekufundisha kazi (Intern Supervisor). Furahia mashauri yake ili uweze kufaidi uzoefu wake. Mama White anasema, “Hebu Watendakazi wa muda mrefu (older workers) wawe waelimishaji, wajitunze wenyewe chini ya nidhamu ya Mungu. Hebu vijana wajisikie ni fursa (privilege) kujifunza chini ya watendakazi wa muda mrefu, na hebu wao wabebe kila mzigo ambao vijana na uzoefu wao vitaruhusu. Kama vile Eliya alivyowaelimisha vijana wa Israeli katika shule ya manabii;vijana leo wanahitaji kuwa na mafunzo kama hayo hayo. Haiwezekani kushauri kwa kila kipengele katika sehemu ambayo vijana wanapaswa kutenda; lakini wanapaswa kuelekezwa uaminifu na watendakazi wa muda mrefu (older workers), na kuwafundisha kumtazama daima Yeye (Yesu) ambaye ni mwenye kuanzisha na kuitimiza imani yetu.”
“Kipindi chote cha ajira kabla mtendakazi mpya (anayeanza kazi) hajawekewa mikono anapaswa inapaswa afikiriwe sana sehemu ya mafunzo yake. Miaka yake miwili ya kwanza, hususani, inapaswa isimamiwe kwa ukaribu zaidi. Msimamizi anapaswa kufikiriwa mtu anayefaa (au mwenye sifa) ya kusimamia asimamie tu mara baada ya kuchukua mafunzo maalumu kama haya yanayotolewa na kozi hii.”
SIRI YA MAFANIKIO KWA MCHUNGAJI UNAPOONGOZA MTAA MKUBWA.
Kanisa la Waadventista Wasabato katika Afrika, Asia, Amerika ya Kusini, n.k wachungaji wake wengi wanaongoza makanisa mengi kutokana na uhaba wa watendakazi na pia hali ya uwezo wa kuajiri au kusomesha watendakazi wapya. Hivyo inalazimu mchungaji kuchunga au kuongoza makanisa kuanzia matatu hadi ishirini na mbili. Jambo ambalo halileti ufanisi kwa mchungaji kuweza kutekeleza majukumu yako kama mchungaji kama vile kuwalisha kiroho, kuwatembelea mshiriki mmoja na kuomba naye, kuendesha huduma za meza ya Bwana, n.k. Hivyo ili kufanikiwa wewe kama mchungaji wa mtaa ya mambo yatakayokusaidia. Nayo kama ifuatavyo:-
1. Wafundishe wazee wa kanisa huduma ya kichungaji (uongozi wa huduma ya kichungaji) na kuwatengeneza wafae kwa uongozi wa kanisa. Wafanye wawe na mzigo wa kulea washiriki, kuhubiri, kufanya uinjilisti, kutoa elimu ya Kikristo, na kutunza mali za kanisa.
2. Ujihusishe katika kila aina ya makusanyiko ya washiriki. Hili linahusu kuwa na ratiba ya ziara zako na mambo yako (itinerary). Unapofika katika kanisa lolote la mtaa wako hakikisha unahudumu siku hiyo maana wazee wa kanisa na washiriki wamekuwa na muda mrefu wa kuhudumiana wakati haupo. Pia mchungaji uwe na ratiba ya dharura panatokea misiba, kuwaona washiriki walio wagonjwa taabani. Ndoa na ubatizo hakikisha unatoa msisitizo wa huduma hizi zipangwe vyema.
3. Toa mafunzo ya ujuzi wa kichungaji kwa viongozi wa kanisa kama vile wazee wa kanisa na mashemasi. Fanya hili kwa vitendo kwa Kuendesha mikutano ya kamati mbalimbali, Namna ya kuandaa hubiri na kulihubiri; utembeleaji wa washiriki wenye ufanisi; Imarisha idara za kanisa; Namna ya utunzaji wa mali za kanisa; Fundisha kwa kina kuuelewa ujumbe wa Kiadventista; na namna ya utunzaji wa waumini wapya.
A. Mwaka 1991 General Conference kikao chake cha mwaka kilipendekeza kuwa “Fildi/Konferensi kuendesha kwa kiwango cha chini Semina moja ya Mafunzo kwa Wachungaji na wazee wa Kanisa kila Mwaka. Ikiwa ni muhimu, makanisa yanapaswa kulipia gharama za usafiri kwa wazee wao kwa kuhudhuria semina hii.”
B. Wachungaji wa Mitaa vile vile wanapaswa kupanga na wazee wote katika mtaa wake kila mwezi au kwa miezi miwili. [Nyongeza yangu: kuwa na kikao cha kupanga kazi yaani baraza la mtaa kutoa semina na mipango ya mtaa wako]. Mikutano hii italenga kupanga mipango kwa mtaa na makanisa. Mipango hii itashughulika na uinjilisti, kufungua maeneo mapya katika mtaa, masomo ya kuhubiri, utembeleaji, magoli ya makanisa na mtaa, ratiba (itenerary) ya mchungaji na mipango yake.
4. Toa hamasa kwa kanisa kuendesha mahubiri na ubatizo wa mara kwa mara. Na pia hamasisha makanisa kuona umuhimu wa kuendesha meza ya Bwana kila robo na pia utoaji wa taarifa kila robo. Toa umuhimu wa makanisa kuwa mikutano ya mashauri kila mara kwa kadiri iwezekanavyo ili kuleta umoja na uwazi kwa mipango ya kanisa.
MAMBO YA FEDHA YA KUZINGATIA.
1. Mchungaji unapaswa kutambua kuwa wewe ni mkaguzi namba moja wa kanisa na pia kumfundisha mzee wa kanisa namna ya kukusaidia kukagua fedha za kanisa. Hakikisha uwe na wivu na mali ya Bwana yaani mlinzi wa hazina ya Mungu. Pitia risiti zote unapoletewa taarifa. Kagua zote na hatimaye ufunge taarifa yako.
2. Nunua kaunta ‘book’ kwa ajili ya kutawala vitabu vyote. Unapopokea vitabu ofisini hakikisha unahakiki namba zote kuwa ziko sawa. Pia unapotoa kitabu hakikisha unamsainisha anayepokea kwa kuandika jina lake, cheo chake kanisani, na tarehe na namba ya kitabu kinachorudi hatimaye namba ya kitabu kinachotoka. Epuka kutoa kitabu kingine bila kupokea kinachoisha.
MAMBO YANAYOMHUSU MKE WA MCHUNGAJI MPYA.
Kazi na mafanikio ya mchungaji ipo nyuma ya mke wake na hata watoto wake. Mwenzi wako anaweza kuifanya kazi yako kuwa ngumu awe rahisi kwa namna anavyohusiana na washiriki. Ikiwa atakuwa mgomvi kila wakati kazi yako itakuwa chungu katika kila mtaa utakaokwenda. Hivyo mama mchungaji anapaswa kuwa mwangalifu sana katika kuisimamisha kazi ya Mungu katika mtaa au mazingira yao.
1. Mke wa mchungaji usiwe na rafiki unayempendelea mtaani au ofisini.
2. Mke wa mchungaji epuka kumsema mke wa mchungaji au mchungaji aliyeondoka kabla yako. Usikubali kumsengenya kwa njia yoyote.
3. Mke wa mchungaji na kwaya ya kanisa. Hakuna ubaya kuwa mwimbaji wa kwaya ya kanisa. Bali tatizo ni pale mke wa mchungaji unaposhindwa kutambua kuwa wewe ni mwimbaji lakini kubwa kupita yote ni mke wa mchungaji. Epuka vikao vya kwaya na mambo ya kwaya yanayoleta upinzani na kanisa au kufanya kinyume na maadili ya kanisa. Uwe na tahadhari katika ushiriki wako katika kwaya maana ni kitendo nyeti ambacho mara zote kinaangaliwa kwa umakini sana (sensitive area).
4. Mke wa mchungaji unapaswa uwe kielelezo katika kuvaa kwako, kujipamba kwa kiasi, na mazungumzo yako. Kumbuka kazi ya mchungaji inakuwa nzuri au mbaya pale mke anapokuwa na mvuto mzuri au mbaya. Omba sana maana Shetani anaweza kukufanya kikwazo cha kazi ya Mungu.
5. Mke wa mchungaji jiepushe kujiingiza katika migogoro inayomhusu mume wako dhidi ya washiriki. Kunapotokea kutokuelewana kati ya mchungaji na uongozi au kanisa kazi yako uliyopewa na Mungu sio kuchochea magomvi bali ni KUOMBA NA KUMFARIJI MUMEO.
Asante kwa ujumbe mzuuuuuuuuuri sana.Mungu akubariki.
ReplyDeletePia naomba kusaidiwa sifa za kujiunga na chuo au kozi ya uchungaji wa kiadventista.
Mungu akubariki sana Pr. Mwanga kwa dondoo hizi adhimu.
ReplyDeleteJaspar Falmeni Mmbaga- Mwanza