JE, KWANINI SIKU YA SABATO NI SIKU YA JUMAMOSI?


Watu mbalimbali wamekuwa wakichanganyikiwa kuhusu siku ya sabato kuwa ni ipi katika juma lakini leo tutaacha vitabu vikuu vya imani nyingi pekee vitupatie ufumbuzi wa jambo hili.
Tuanze na biblia Mungu anasema mahali fulani kuwa sabato ni siku ya saba, Kutoka.20:8-11, “Ikumbuke SIKU YA SABATO uitakase. Siku sita fanya kazi utende mambo yako yote; lakini SIKU YA SABA NI SABATO YA BWANA, Mungu wako siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako. Wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako.  Maana, kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe SIKU YA SABA; kwa hiyo BWANA akaibarikia siku ya sabato akaitakasa.” Hapa tunaona kuwa siku ya SABA NI SABATO ya BWANA MUNGU, hivyo katika juma moja la siku sita basi siku moja ni sabato ya BWANA. Katika siku hiyo Mungu anasema usifanye kazi yako yo yote wewe, mali zako hata watu wa nyumbani kwako.
Lakini je, katika juma siku ya saba ni ipi? Au kwa maana nyingine siku ya sabato ni ipi? Biblia inatoa jibu kuwa sabato ni SIKU YA JUMAMOSI, Mathayo.28:1,5 inasema “Hata SABATO ilipokwisha, ikipambazuka SIKU YA KWANZA ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu Yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi. Malaika akawajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa. Hayupo hapa; kwani AMEFUFUKA kama alivyosema.” Kumbe sabato yaani siku ya saba ni siku inayotangulia kabla ya siku ya kwanza ya juma. Katika biblia ya Kiswahili cha kisasa ya habari njema fungu hili linasomeka vizuri kabisa kuwa “Baada ya SABATO, karibu na mapambazuko ya SIKU ILE YA JUMAPILI, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kutazama lile kaburi.” Hapa biblia inaonesha kuwa siku ya sabato ni siku moja kabla ya Jumapili, maana sabato ikiisha jumapili huanza. Je, siku hiyo ni ipi? Jibu ni rahisi sana nalo ni JUMAMOSI.
Hadi leo, watu wote wanajua kuwa Yesu aliteswa na kufa siku ya Ijumaa, akalala kaburini siku ya Jumamosi na Jumapili akafufuka. Siku hii ya mateso na kifo cha Yesu inaitwa IJUMAA KUU, ni siku ya IJUMAA. Kipindi kile siku hii iliitwa SIKU YA MAANDALIO YA SABATO, Luka. 23:53-54 “Akaushusha(mwili wa Yesu), akauzinga sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililochongwa mwambani, ambalo hajalazwa mtu bado ndani yake. Na SIKU ILE ILIKUWA SIKU YA MAANDALIO, na SABATO ikaanza kuingia.” Hivyo siku moja kabla ya Sabato inaitwa siku ya Maandalio yaani Ijumaa nayo ilikuwa siku ya kujiandaa maana siku ya sabato hawakufanya kazi yoyote. Biblia ya Kiswahili cha kisasa ya habari njema inasema, “Siku hiyo ilikuwa IJUMAA, na maandalio ya siku ya SABATO yalikuwa yanaanza”. Kwahiyo sabato ni siku iliyo katikati ya IJUMAA NA JUMAPILI ambayo ni Jumamosi si ndiyo?
Hata Kurani nayo inashuhudia kuwa sabato ni siku ya saba yaani Jumamosi nayo inatakiwa kutumika kwajili ya ibada, katika surat Al-Baqarah(2) kifungu sha 65 imendikwa; “Na kwa yakini mmekwisha kujua khabari za)  wale walioasi miongoni mwenu katika (amri ya kuihishimu) jumamosi. Basi tukawaambia: “kuweni manyani wadhalilifu”. Hapa tunaona kuwa Kurani inasema siku ya jumamosi ni siku inayotakiwa kuheshimiwa na kutofanya hivyo ni uasi yaani ni dhambi. Pia surat Al-Aaraf(7) kifungu cha 163a inakazia kuwa “Na waulizeni habari za mji ambao ulikuwa kando ya bahari;(watu wa mji huo) walipokuwa wakivunja (sheria ya) Jumamosi (ambayo waliambiwa wasifanye kazi katika siku hiyo, wafanye ibada tu.” Hapa tunaona Kurani ikiunga mkono biblia kwamba siku ya sabato yaani jumamosi ni siku ya kutofanya kazi kabisa bali ni siku ya kufanya ibada tu.
Nawe msomaji wa ujumbe huu haijalishi imani yako ni ipi au itikadi yako ni ipi Biblia na Kurani vinakutaka leo urudishe utukufu wa Bwana katika sabato yake takatifu siku ya Jumamosi wala si katika siku nyingine yoyote. Nenda katika kanisa lolote jumamosi ya juma hili, uungane na waabuduo halisi wamwabuduo Mungu katika Roho na Kweli.
Na MUJAYA MUJAYA, 0767578122.

0 comments: